Jumatatu 2 Novemba 2026 - 22:00
Kwa nini hatupaswi kutumia neno «Wahouthi» kuwataja wananchi wa Yemen?

Hawza/ Kurudiwa matumizi ya jina «Wahouthi» katika vyombo vya habari vya kimataifa kumeanza, hatua kwa hatua, kulifanya jina hilo kuwa mbadala wa kuwataja wananchi wa Yemen, taasisi zake za kisiasa na vikosi vyake vya kijeshi. Mwelekeo huu, ambao unavuka mipaka ya uchaguzi wa maneno tu, unaathiri namna hadhira inavyofahamu nchi hiyo na matukio yanayoendelea ndani yake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, makala hii inachunguza sababu na matokeo ya matumizi ya jina «Wahouthi» katika simulizi za vyombo vya habari kuhusu matukio ya Yemen.

Katika vita vya usimuliaji na uwasilishaji wa matukio, wakati mwingine, kabla hata ya ukweli kupotoshwa, maneno ndiyo hubadilishwa. Uchaguzi wa jina linaloonekana kuwa rahisi unaweza kujenga taswira tofauti kuhusu nchi, taifa na matukio yake ya kisiasa katika fikra za hadhira. Mojawapo ya mifano inayostahili kuzingatiwa kuhusu suala hili inaonekana katika namna vyombo vya habari vinavyoripoti matukio ya Yemen. Katika hali hiyo, baadhi ya vyombo vya habari na viongozi wa kisiasa, badala ya kutumia majina kama «Serikali ya Yemen», «Wananchi wa Yemen» au «Vikosi vya Wanajeshi vya Yemen», hutumia neno «Wahouthi»; kana kwamba nchi nzima pamoja na jamii yake inaweza kufupishwa na kuwakilishwa kwa jina la harakati moja ya kisiasa.

Namna hii ya utoaji majina imejitokeza zaidi katika uripoti wa misimamo ya Yemen kuhusu Palestina, vita vya Ghaza, kukabiliana na utawala wa Kizayuni na matukio ya Bahari ya Shamu. Katika ripoti nyingi, hatua zinazotangazwa au kutekelezwa na Vikosi vya Wanajeshi vya Yemen huwasilishwa kwa kauli kama vile «Wahouthi wametishia» au «Wahouthi wamelenga meli»; ilhali katika hali nyingi, suala linalozungumziwa linahusu msimamo rasmi wa taasisi zilizopo Sana’a au operesheni za Vikosi vya Wanajeshi vya nchi hiyo.

Neno «Mhouthi» limetokana na jina la ukoo la Hussein Badruddin al-Houthi, mwanzilishi wa Harakati ya Ansarullah, na hutumiwa katika maandiko ya kihistoria na kisiasa kuirejelea harakati hiyo. Kwa hiyo, kutumia jina hilo mahsusi kuitambulisha Harakati ya Ansarullah si jambo lisilo sahihi wala la kumdhalilisha. Tatizo hujitokeza pale ambapo neno hilo linapotumiwa badala ya jina la nchi, wananchi wake au taasisi zake za kiserikali, na matukio yote ya Yemen yanapohusishwa na harakati moja ya kisiasa.

Mojawapo ya matokeo ya utoaji majina wa aina hii ni kuipunguza harakati ya kisiasa na kijamii na kuifungamanisha na jina la ukoo mmoja. Katika kipindi chote cha shughuli zake, Harakati ya Ansarullah imegeuka kuwa harakati yenye muundo wa kisiasa, taasisi, mitazamo na wafuasi wake katika jamii. Matumizi ya mara kwa mara ya jina «Wahouthi», hasa linapotumika badala ya jina la harakati hii, yanaweza kujenga taswira kwamba kinachozungumziwa ni kundi dogo linalohusishwa na familia moja, badala ya harakati ya kisiasa ambayo imekuwa na nafasi yenye ushawishi katika matukio ya Yemen katika miongo kadhaa iliyopita. Namna hii ya utoaji majina humfanya msomaji asione kwa uwazi ugumu wa mchakato wa kuundwa na kupanuka harakati hii pamoja na mazingira ya kijamii yaliyochangia uwepo wake.

Kwa upande mwingine, maneno katika mazingira ya vyombo vya habari huwa hayabebi maana moja katika kila matumizi yake. Jina «Wahouthi» katika baadhi ya ripoti linaweza kutumiwa tu kuirejelea Ansarullah; hata hivyo, linapounganishwa na misemo kama vile «wanamgambo wa Kihouthi», au linaporudiwa mara kwa mara sambamba na maneno yenye maana hasi, linaweza kugeuka kuwa nyenzo ya kuweka lebo na kujenga taswira hasi kuhusu harakati hiyo. Katika aina hii ya usimulizi, kabla hata hadhira haijafahamu misimamo, utendaji na sababu za harakati hiyo, tayari hukumu fulani huanza kujengeka katika fikra zake.

Jambo jingine ni athari za lugha hii katika namna msingi wa kijamii wa Harakati ya Ansarullah unavyowasilishwa.

Wakati harakati moja inapotambulishwa mara kwa mara kwa kutumia jina la ukoo la mwanzilishi wake, inaweza kujengeka dhana kwamba shughuli na ushawishi wake vinaishia katika mduara mmoja wa kifamilia au kundi dogo tu. Hali ambayo, ili kufahamu nafasi ya harakati yoyote ya kisiasa, ni lazima kuzingatia pia historia yake, muundo wake, wafuasi wake na mazingira ya kijamii yaliyochangia kuibuka kwake. Bila shaka, jambo hili halimaanishi kwamba mitazamo ya wananchi wote wa Yemen inafanana na ile ya Ansarullah; kama ambavyo haiwezekani pia kupuuza upinzani wa sehemu fulani ya jamii dhidi ya harakati hiyo.

Kuenea kwa jina hili katika vyombo vya habari vya Magharibi na baadhi ya vyombo vya habari vya Kiarabu pia kumekuwa na mchango katika kuimarisha taswira ya aina hiyo. Wakati msemo mmoja unapogeuka kuwa istilahi inayotawala katika uripoti wa mgogoro fulani, vyombo vingine vya habari vinaweza pia kuiga mtindo huo, hata pale ambapo kuna majina sahihi zaidi ya kuelezea tukio au taasisi inayohusika. Kwa namna hiyo, uchaguzi mmoja wa msamiati, hatua kwa hatua, hugeuka kuwa mfumo uliozoeleka wa kusimulia matukio; mfumo ambao si lazima uakisi nyanja zote za uhalisia.

Hata hivyo, ni lazima kutofautisha baina ya matumizi mbalimbali ya neno hili, ikiwa mada ya habari inahusu mahsusi msimamo au hatua ya Harakati ya Ansarullah, kutumia jina la harakati hiyo au jina lake linalotambulika kunaeleweka. Lakini ikiwa habari inahusu wananchi wa Yemen, taasisi za kiserikali zilizopo Sana’a au Vikosi vya Wanajeshi vya nchi hiyo, kubadilisha majina yote hayo na kuyaita «Wahouthi» kunapunguza usahihi wa kitaaluma katika uandishi wa habari.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha